Usiku wa Epiq Night ndani ya Maisha
Club utakuwa ni usiku wa kukumbukwa kwa wapenda burudani wengi hasa baada ya
wasanii walioshiriki shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search kutoa
burudani ya aina yake.
Katika usiku huo ambao ukumbi wa
Maisha ulikuwa umejaza wapenda burudani na wadau mbalimbali wa muziki,
ulishuhudia vijana hao wakiimba kwa mara ya kwanza mbele ya wakazi wa Dar es
Salaam tokea walipoimba mara ya mwisho wakati wa fainali za EBSS pale Diamond
Jubilee.
Wasanii hao wakiwa bado wana moto
kutokea burudani waliyoitoa Dodoma wiki mbili zilizopita, walifanya mashabiki
waliojazana Maisha kushidwa kukaa na kushangilia wakati wote.
Burudani hiyo ilifunguliwa na mkali
wa Bongo fleva Rich Mavoko, akifuatiwa na kijana kutoka BSS, Vincent aliyeimba
wimbo wake wa INYE NA IWE.
Ufunguzi huo, ambao ulifanya ukumbi
mzima kupiga mayowe, ulizidi kupamba moto baada ya kijana toka Dodoma, Godfrey
Levis alipopanda na kibao chake cha MAYA.
Shangwe zilizidi pale malkia kutoka
THT, Linah alipopanda jukwaani kuimba nyimbo zake kali kama Oliva Twist na
Nshafahamu kabla ya kumkaribisha jukwaani, dada mwenye sauti kali, Nsami kuimba
wimbo wake wa MUONGO.
Ilibidi nguvu ya ziada itumike
kuwadhibiti mashabiki pale alipopanda dada wa Taarab, Husna, ambapo uchezaji
wake na kumiliki jukwaa kuliwafanya mashabiki kutaka kupanda jukwaani kumtuza
wakati akiimba wimbo wake unaofanya vizuri, NAWAMIMINA.
Huku mashabiki wakizidi kushangilia
kwa nguvu, dada mwingine aliyejizolea umaarufu kwa kuimba nyimbo za
kiutamaduni, Nshoma, akapanda kuimba wimbo wake wa ‘MAMA AFRIKA’ ambapo
uliwakonga mashabiki kwa midundo yake.
Kama hiyo haitoshi, mashabiki
walizidi kushangilia pale mwimbaji bora wa kiume, Barnaba alipopanda kuimba
nyimbo zake za Sorry na Magube gube.
Ilikuwa burudani baada ya burudani
baada ya Barnaba kumkaribisha jukwaani mwanadada mwingine anayefanya vizuri na
wimbo wake wa DREAM TONIGHT, Menina ambaye aliufanya ukumbi kumshangilia kwa
uwezo wake mkubwa wa kutawala jukwaa.
Alikuwa ni Norman, aka we mbaya,
aliyefanya mashabiki kujazana stejini alipopanda kuimba wimbo wake wa ‘SI
WEWE’. Norman ambaye kutolewa kwake kwenye EBSS kuliwasikitisha wengi, alifanya
show ambayo wengi walizidi kuamini kwamba alistahili kufika mbali.
Hadi wakati mshindi wa tatu wa
shindano la EBSS, Wababa Mtuka anapanda jukwaani kuimba kibao chake cha ‘My
Wife’ na Kitorondo mashabiki walikuwa bado wakishangilia namna alivoonyesha
uwezo katika kuimba na kucheza.
Wa mwisho kabla ya mshindi wa milioni
hamsini kupanda alikuwa ni mkali wa RNB Tanzania, na mshindi wa tuzo za kili,
Ben Paul, ambaye aliwakonga nyoyo mashabiki wake kwa nyimbo zake kali kama Pete
na Samboira kabla ya kumkaribisha jukwaani Walter.
Mashabiki hao waliokuwa wakimsubiri
kwa hamu, walianza kupiga kelele Walter Walter, kabla ya kuwatuliza kwa kuimba
wimbo wake mpya wa ‘Siachi’ akifuatiwa wimbo wake mwingine wa ‘Mamy Love’ pamoja
na ‘RINGA’.
Walter alipata wakati mgumu jukwaani
ambapo mashabiki walimuomba azirudie nyimbo zake zaidi ya mara tatu hali
iliyoonyesha kukubalika kwa hali ya juu.
Mashabiki wengi wakizungumza baada ya
burudani hiyo walionyesha kuwakubali vilivyo wasanii wa EBSS, huku
wakiwatabiria makubwa.
‘Hakika vijana wana vipaji na wanajua
hasa kutoa burudani, wakipewa sapoti watafika mbali sana’ alisema Jumanne Sally
mmoja wa mashabiki aliyehudhuria burudani hiyo.
Ziara hiyo ya washindi wa Epiq BSS
inaelekea Mtwara baada ya wiki mbili.
No comments:
Post a Comment